Tuesday, 7 January 2014

WASANII WA FILAMU WAUZIWA STIKA KWA PAUNI YA ENGLAND, TRA YAJIKANGANYA, WIZARA HAIJUI.

Tasnia ya sanaa imeendelea kuandamwa na changamoto nyingi ikiwamo wasanii kununua stika za kazi zao kwa pauni ya Uingereza badala ya shilingi ya Tanzania.


Mfumo huo wa ununuaji wa stika zinazobandikwa katika makasha ya kazi zinazoandaliwa na wasanii hao hutolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ambayo imethibitisha jambo hilo, huku ikieleza kuwa wanauza kwa pauni kwa sababu mtengenezaji wa stika hizo akaunti yake ipo mwenye pauni, siyo shilingi.
Wakizungumza na MWANANCHI kwa nyakati tofauti wasambazaji wa kazi hizo, wasanii na uongozi wa sanaa nchini walisema tangu kuanza rasmi kwa mfumo huoJulai 2013, kumekuwa na hali ya sintofahamu kutokana na stika hizo kuwa adimu na zinapopatikana kuuziwa kwa fedha za nje kinyume na makubaliano ya serikali na wasanii juu ya mfumo huo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), Simon Mwakifamba alisema stika hizo kuuzwa kwa pauni ni changamoto mpya inayoukumba mfumo wa urasimishaji wa kazi za wasanii na kupoteza maana nzima ya zoezi hilo.
“Limekuwa ni tatizo kubwa linalowakwaza wasanii nchini hasa wasambazaji wa kazi hizo kutokana na gharama kubwa wanayotumia sambamba na kukosa stika kwa wakati mwafaka,” alisema na kuongeza;
“Mtu umeshajipanga kutoa kazi ziku mbili kabla,  ukienda  TRA unaambiwa stika zimekwisha wakati tayari  umeshachukua mkopo benki yaani unakuwa umeongeza matatizo mengine juu.”
Mwakifamba alitoa wito kwa serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha inarekebisha mfumo huo uliopo sasa ambao umeonekana kuwa kero  kwa wasanii.
“Naona kutumia pauni ni kuongeza gharama kubwa ambayo isingeweza kufikiwa iwapo stika hizi zingeuzwa kwa fedha ya Tanzania.
“Kwa mujibu wa kiongozi wetu sidhani kama haya ndiyo yalikuwa makubaliano yetu. Stika moja tunanunua kwa shilingi 14, lakini unalipa kwa pauni na si shilingi ya Tanzania, hata hivyo tunauziwa kuanzia stika 100 na si chini ya hapo.”
Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema, “Kubwa zaidi tunalolalamikia sisi kama wasambazaji na wasanii ni kuuziwa stika hizi kwa fedha isiyo yetu, kwa nini iwe hivi, pauni kila siku inabadilika mara inapanda mara inashuka.”
Novemba alisema, “Wasanii wa muziki wanalalamika kuhusu hilo hasa wa muziki wa Injili. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wameamua kukacha kabisa albamu kutokana na ukweli kwamba hawauzi, lakini hata waliofurahia urasimishaji bado utata unakuja kwenye stika yaani hakuna afadhali tulidhani tutapata haki, lakini sasa mambo ndivyo sivyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Five Effect, kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa kazi za wasanii, William Mtitu naye alisema, “Kuna uhaba wa stika hata hivyo tunanunua kwa pauni, wasanii tuliamua kusambaza kazi zetu wenyewe kutokana na tatizo la kutoendelea na Mhindi anatunyanyasa siyo siri akinunua kazi yako humdai tena anaitumia atakavyo.


Kigogo TRA ahamaki
Katika hali ya kushangaza Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alikana tuhuma hizo na kudai kwamba si kweli bali wasanii wanauziwa stika hizo kwa shilingi za Tanzania.
“Taarifa hizo hazina ukweli wowote, stika zote zinazouzwa hapa TRA zinauzwa kwa mfumo wa fedha za Tanzania na si fedha za kigeni, hatujawahi kuwauzia wasanii stika kwa fedha za Uingereza (pauni), waambie hao wanaosema hivyo wakuonyeshe risiti walizolipia kwa pauni.”
Kauli ya wasambazaji
Uongozi wa Kampuni ya Steps Entertainment ambao ndio wasambazaji wa kazi za wasanii walipotakiwa kuonyesha risiti ambazo walilipia stika hizo kwa pauni badala ya shilingi ulisema, “Ni jambo la kushangaza kama TRA wenyewe wanatulipisha kwa pauni kisha wanakana haiwezekani, risiti tunazo ila zungumza na Afisa Utafiti Mwandamizi wa TRA.”
TRA yathibitisha
Ofisa Utafiti Mwandamizi wa TRA, Ephraim Mdee alithibitisha matumizi ya pauni ya Uingereza katika ununuzi wa stika za wasanii na kutoa maelezo ya kwa nini mamlaka hiyo iliamua kutumia pauni  badala ya fedha za Tanzania.
“Ni kweli wasanii wanauziwa stika kwa pauni ya Uingereza. Tulifanya hivi tukiwa na makusudi maalum kwa kawaida stika hizi tunazinunua kutoka kampuni ya M/S Hague Cheque Security na stempu moja inatengenezwa kwa pauni 0.00285,” alisema na kuongeza;
“Lakini gharama hii ukiigawanya kwa shilingi ya Tanzania unapata shilingi 7 na hii unazidisha mara mbili na kupata shilingi 14. Tuliamua kutumia pauni kutokana na tatizo la kupanda na kushuka kwa fedha hiyo hata hivyo mtengenezaji akaunti yake ipo kwenye pauni,” alisema Mdee.
Mdee alisema kuhusu suala la kutokuwepo stika kwa wakati, ni tatizo lililojitokeza siku za awali baada ya kuanzishwa mfumo huo.  “Nadhani hicho ni kitu cha kawaida, inawezekana mteja akaja na kununua nyingi.”
Wizara
Waziri wa Biashara na Viwanda, Abdallah Kigoda alishangazwa na taarifa hizo huku akisisitiza kwamba hayakuwa makubaliano yaliyopitishwa na bunge.

 “ Hili ni jambo nyeti na wizara yangu inaanza kulishughulikia haraka sana. Nakiri kwamba Wizara ya Fedha inapaswa kuangalia suala hili kwa umakini zaidi kwani wizara yangu haijalipitisha hilo na ninashangazwa kwa nini wasanii wanunue stika hizi kwa pauni?” alihoji Kigoda.

credit: Mwananchi

                                               Baadhi ya wasanii wa filamu nchini

No comments:

Post a Comment